Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Ihaab Hamade, mbunge na mjumbe wa kambi ya Uaminifu kwa Muqawama, katika hotuba yake aliyotoa kwenye hafla iliyofanyika katika Mkusanyiko wa Hazrat Sayyid al-Shuhadaa (a.s) katika mji wa Hermel, kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mwaka wa kwanza ya kuuawa kishahidi kwa Hassan Muhammad Al-‘Amiri, alisisitiza kwa kusema: Sisi ni watu ambao hatushtushwi na vitisho. Endapo adui wa Kizayuni atataka kuongeza kiwango cha mashambulizi yake au kuanzisha vita vikubwa, basi anapaswa kujua kuwa haya si matembezi ya bustanini; bali ni vita vyenye gharama na bei kubwa.
Aliongeza kwa kusema: Wakati adui alipowatishia wakazi wa mji wa mpakani wa Bait Lif (ulio kwenye mpaka wa Lebanon na Palestina inayokaliwa kwa mabavu), watu wa mji huo hawakuonesha woga wowote; bali athari ya onyo hilo iligeuka kinyume — walioshtuka na kuitikia walikuwa ni walowezi wa Kizayuni. Kiwango cha uwepo wa walowezi katika makazi ya kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu kimeshuka hadi chini ya asilimia 50; waliogopa, walipiga mayowe na wakaanza kuyahama makazi yao kuelekea ndani zaidi ya ardhi inayokaliwa.
Mjumbe wa kambi ya Muqawama alisema: Asipatikane yeyote wa kuwahadaa kwa vitisho na kuwavunja mori; muqawama wetu ni imara na una nguvu. Maelfu ya wapiganaji waliotayari kwa shahada kama shahidi Haj Hassan Al-‘Amiri wapo, kama alivyobainisha shahidi kamanda Haitham Al-Tabtaba’i — yule ambaye baada ya miaka 25 ya harakati za muqawama, alilengwa mara nyingi kwa njama za kuuawa na adui, lakini akaokoka risasi za adui huko Lebanon, Syria, Iraq na Yemen. Yeye pamoja na ndugu zake Haj Imad, Sayyid Mohsen na Haj Abdulqadir, waliofanya miradi ya Kimarekani ishindwe.
Hamade aliendelea kusema: Wakati Sheikh Na’im Qassem, Katibu Mkuu wa Hezbollah, aliposema kuhusu “siri ya uhai wa muqawama”, alikusudia kuwa maelfu ya wapenzi wa shahidi kamanda Al-Tabtaba’i bado wako hai na wanafanya kazi kikamilifu katika njia ya kutekeleza malengo ya muqawama.
Alirejea katika kikao cha hivi karibuni cha Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri na kundi la wabunge wa Lebanon na kusema: Katika kikao hicho, waziri wa Misri alizungumza kwa lugha ya vitisho akisema vita viko karibu, kana kwamba anataka kutuambia tulazimike kupiga magoti mbele ya adui wa Kizayuni, tusalitiwe na kutelekeza uhuru wetu, rasilimali zetu na heshima yetu.
Hamade aliongeza: Wamarekani nao wanatuma wajumbe wao ili kuongeza kiwango cha vitisho. Lakini swali ni hili: kama adui angeweza kufikia malengo yake, kwa nini alisaini makubaliano ya kusitisha mapigano huku bado alikuwa anaendelea na operesheni za kijeshi? Ukweli ni kwamba hakufikia lengo lolote lile. Lengo kuu la Israel lilikuwa kuuangamiza Muqawama na Hezbollah; je, alifanikiwa kutimiza lengo hilo?
Mjumbe wa kambi ya Muqawama alisisitiza: Israel inadhani inaweza kwa nguvu kuondoa silaha za Muqawama; lakini je, ina uwezo wa kufanya hivyo? Iliingia Ghaza katika eneo lenye ukubwa wa takribani kilomita za mraba 300 pekee, lakini imeshindwa kulitatua tatizo la Ghaza; imeshindwa pia katika faili la Yemen, Iran, na Lebanon. Mafaili yote haya bado yapo wazi, na haikufanikiwa katika hata moja.
Mwisho wa hotuba yake, Hamade aliwahutubui baadhi ya wakosoaji wa ndani ya Lebanon kwa kusema: Wale wanaouliza kwa nia ya uhasama kwamba Iran imefanya nini, heri wawatazame Waisraeli wenyewe, vyombo vya habari vya Magharibi, na yale yaliyonukuliwa kutoka kwa rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump — jinsi alivyofanya upatanishi wa kusimamisha vita kwa hofu kwamba endapo vita vingedumu kwa muda mrefu, Israel ingeangamia kutoka ndani.
Maoni yako